Uchunguzi wa DNA uliofanyiwa miili 21 ya wanafunzi waliofariki kwenye mkasa wa moto katika shule ya Hillside Endarasha Academy umekamilika na miili hiyo kutambuliwa.
Akithibitisha hayo, Mpasuaji Mkuu wa maiti wa serikali Johansen Oduo, amesema mchakato wa kuwajulisha wazazi wa wanafunzi hao umeanza, ukiongozwa na maafisa wa idara ya makosa ya jinai (DCI), Shirika la Msalaba Mwekundu na maafisa wa kutoa ushauri nasaha.
“Tumepokea matokeo ya uchunguzi wa DNA uliofanyiwa wanafunzi wa shule ya Endarasha, na miili yote imetambuliwa,” alisema Oduor.
Ameongeza kuwa mikakati maalum imewekwa kuwawezesha wazazi kutazama miili hiyo, huku shughuli hiyo ikifanikishwa na maafisa wa shirika la msalaba mwekundu na watoaji ushauri nasaha.
Wakati huo huo, kaimu kamishna wa kaunti ya Nyeri Pius Murugu amesema ibada ya pamoja ya wafu itaandaliwa katika uwanja wa Mweiga kabla ya miiili hiyo kukabidhiwa familia zao kwa ajili ya mazishi.
Wanafunzi hao waliangamia baada ya moto kuteketeza bweni lao mapema mwezi Septemba.