Miili ya waliofariki Shakahola kutolewa kwa familia wiki ijayo

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali kuanzia wiki ijayo itaanza kutoa miili ya waathiriwa wa mauaji ya Shakahola kwa familia zao kwa ajili ya mazishi.

Haya ni kwa mujibu wa mpasuaji mkuu wa serikali Johansen Oduor.

Oduor aliyekuwa akihutubia wanahabari katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi leo, alielezea kwamba zoezi hilo litaanza Jumanne, Machi 26, 2024.

Kulingana na Oduor, mkemia mkuu wa serikali amefanikiwa kutambulisha miili 34 na familia zao kati ya miili yote 428 iliyofukuliwa kutoka kwenye msitu wa Shakahola katika awamu nne.

Daktari Oduor ambaye alikuwa ameandamana na mkuu wa kitengo cha mauaji katika idara ya upelelezi wa jinai Martin Nyuguto, alisema familia zilizotambuliwa zimejuzwa na kwamba watapatiwa ushauri nasaha kabla ya kupokezwa miili hiyo.

Watu hao watahitajika kuwa na barua kutoka kwa machifu wa maeneo yao na waliotoa sampuli za DNA kabla ya kupatiwa miili ya wapendwa wao.

Miili ambayo haitachukuliwa na wenyewe baada ya muda fulani itazikwa na serikali kulingana na sheria. Maziko hayo Oduor alisema yatafanywa kwa njia ambayo itarahisisha ufukuzi iwapo familia zitajitokeza baadaye.

Awamu ya tano ya ufukuzi katika msitu wa Shakahola inatarajiwa kuanza punde baada ya shughuli ya kutoa miili kwa familia hizo, kulingana na Oduor.

Anasema kwamba makaburi mengine 30 yametambuliwa humo kwa ajili ya awamu hiyo.

Share This Article