Mwanamuziki wa Uganda Mickie Wine ambaye ni ndugu ya mwanamuziki na mwanasiasa Bobi Wine ameelezea sababu ya kuhudhuria na kuhusika kwenye mazishi ya mama ya hasimu wake Gravity Omutujju.
Wasanii hao wawili wamekuwa washindani katika ulingo wa muziki kwa muda mrefu ambapo huwa wanatupiana maneno makali na hata kuandaa matamasha siku moja kwenye maeneo yaliyo karibu.
Lakini Mickie alisimama na Omutujju mamake alipofariki ambapo alihudhuria hafla ya mazishi iliyoandaliwa Jumatatu Oktoba 21, 2024.
Wasanii wengine wengi wa Uganda pia walihudhuria hafla hiyo.
Mickie alitoa rambirambi zake na hata alihusika kwenye kujaza udongo kwenye kaburi la mama huyo.
Msanii huyo alielezea kwamba alifika kwenye hafla hiyo kutoa heshima zake za mwisho kwa mama huyo kwa sababu hakuwa na tatizo naye.
“Mtu akikutukana sio lazima umtukane. Kupoteza mzazi ni mojawapo ya mapigo mabaya zaidi kwa mtu. Sikuwa na shida yoyote na mamake.” alisema Mickie kwenye mahojiano na kituo cha runinga cha Spark.
Bobi Wine naye alitoa rambirambi zake kupitia akaunti za mitandao ya kijamii ambapo aliandika, “Nimefahamishwa kuhusu kifo cha Maama Jane Kajoina, mamake ndugu yetu Gerson Wabuyu maarufu kama GRAVITTY OMUTUJJU. Ninatuma salamu zangu za pole kwako na kwa familia yako.”