Mashindano ya michezo kati ya wabunge wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanaendelea katika uwanja wa Pele jijini Kigali nchini Rwanda.
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetangula aliongoza timu ya Kenya kwenye michezo hiyo inayoandaliwa kati ya Disemba 7 na 19, 2023.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi ya awamu ya mwaka huu ya mashindano hayo, Wetangula alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kuimarisha umoja katika mataifa ya Afrika mashariki.
Aliomba wabunge wanaohusika kwenye michezo hiyo waongoze katika kukuza umoja wa kanda wanapotekeleza majukumu yao ya kuwakilisha wananchi na kuunda sheria.
“Ni ndoto yangu kwamba tutashuhudia uunganishwaji wa kanda hii kikamilifu, katika maisha yetu tukiwa na sarafu ya pamoja, mfumo mmoja wa elimu, shirika la pamoja la uchukuzi wa ndege na usafiri huru wa wananchi katika kanda nzima.” alisema Wetangula.
Kiongozi huyo alitambua kwamba kuna vijana wengi sasa katika uongozi akitumai kwamba wataongoza vyema ajenda ya kuunganisha kanda ya Afrika Mashariki.
Aliomba wachezaji wote kucheza kwa uadilifu wakikumbuka kwamba ni ushindani wa burudani tu na wala sio uhasama.
Mashindano ya michezo ya wabunge Afrika Mashariki yalibuniwa mwaka 2001, kama mojawapo ya njia za kuhimiza utangamano na huwa inaandaliwa katika nchi tofauti kila mwaka.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC endelevu, ya amani na inayohusisha wote”.