Mhubiri mmoja katika eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu, amefunguliwa mashtaka katika mahakama moja ya Nakuru kwa madai ya ubakaji na dhuluma za kimapenzi.
Peter Kimondo Baragu almaarufu nabii Peter wa kanisa la Christ Impact Church mtaani Ruiru, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Ruth Kefa katika Mahakama ya Nakuru siku ya Jumatatu.
Mahakama ilifahamishwa kuwa mnamo tarehe May 27, 2022 saa tatu usiku katika mtaa wa White House,kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki, kaunti ya Nakuru, mshukiwa huyo alijaribu kushiriki ngono na mwathiriwa bila idhini ya mwathiriwa.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Daniel Wakasyaka,walipinga kuachiliwa kwa mshukiwa na dhamana, ukitaja huenda akavuruga ushahidi.
Mhubiri huyo anadaiwa kuenda mafichoni baada ya kutekeleza uovu huo, na kusababisha mahakama kutoa kibali cha kukamatwa kwake Machi 1, 2025.
Hata hivyo mshukiwa huyo alkanusha mashtaka hayo na alizuiliwa kusubiri kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iwapo ataachiliwa kwa dhamana, itakayosikizwa Machi 18,2025.