Vyama vya walimu vya KUPPET na KNUT kaunti ya Embu,vimeshikilia kuwa mgomo wa walimu katika eneo hilo ungalipo, kuanzia Agosti 26, 2024.
Katika mkutano wa pamoja siku ya Alhamisi, viongozi wa vyama hivyo kaunti ya Embu, walionya kuwamwanachama yeyote ambaye hatashiriki mgomo huo, atachukuliwa kuwa msaliti.
Aidha viongozi hao waliwashauri wazazi kutowapeleka watoto wao shuleni, muhula wa tatu utakapoanza siku ya Jumatatu.
“Tunawaagiza walimu wote kusalia nyumbani, hadi watakaposhauriwa,” alisema katibu mtendaji wa KNUT Josphat Kathumi.
Baadhi ya maswala ambayo wanalalamikia ni kutopandishwa vyeo kwa walimu 130,000 walioorodheshwa mwaka 2023, kuchelewa kuajiriwa kwa walimu 20,000, kutoajiriwa kwa walimu 46,000 wa JSS kwa masharti ya kudumu na kutowasilishwa kwa matozo wanazokatwa.
“Tunawahimiza wawakilishi wa vyama vya walimu kuhakikisha walimu hawafiki shuleni kuanzia Agosti 26,2024 hadi watakaposhauriwa baadaye,” alisema katibu mtendaji wa KUPPET kaunti ya Embu Rogers Murimi.