Mgomo wa wahadhiri waendelea huku ahadi ya serikali ya ufadhili ikiwa haijulikani

Marion Bosire
2 Min Read
Julius Melly, Mwenyekiti wa kamati ya elimu bungeni

Mgomo unaoendelea wa wahadhiri wa vyuo vikuu hauonyeshi dalili zozote za kukoma, huku kujitolea kwa serikali kufadhili mapatano ya shilingi bilioni 4.3 kukighubikwa na kutojulikana.

Kamati ya elimu katika bunge la taifa inawasaili Constantine Wasonga Opiyo katibu mkuu wa kitaifa wa chama cha wahadhiri UASU na Fred Simiyu Barasa, mwenyekiti wa jukwaa la mabaraza ya vyuo vikuu nchini IPUCCF ili kuangazia suala hilo.

Wabunge walidhihirisha wasiwasi kuhusu athari za mgomo huo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na ukosefu wa ushahidi kuhusu ahadi ya kifedha ya serikali.

Mheshimiwa Rebecca Tonkei, alishangaa ni kwa nini hakuna linaloendelea katika kusuluhisha mgogoro uliopo akisema wamekasirishwa na kuteseka kwa wanao.

“Kamati hii inataka kusuluhisha suala ambalo limekwamisha nchi na wanafunzi wetu.” alisema mheshimiwa Nabii Nabwera.

Maswali yaliibuliwa na mwenyekiti wa kamati ya elimu bungeni Julius Melly kuhusu uhalisia wa stakabadhi zilizowasilishwa na IPUCCF, hasa zinazogusia ufadhili wa shilingi bilioni 4.3.

Barasa mwenyekiti wa IPUCCF, alielezea kwamba ufadhili huo ulizungumziwa katika kiwango cha kamati ya mawaziri mbali mbali baada ya mazungumzo na UASU na IPUCCF kugonga mwamba.

Hata hivyo wanachama wa kamati hiyo hawakushawishika na maelezo hayo wakitaka stakabadhi halisi kutoka kwa serikali kudhibitisha kujitolea kwake kuongeza ufadhili.

Mbunge wa kaunti ya Nyamira Jerusha Momanyi alisema kwamba barua ya hivi maajuzi kutoka kwa katibu wa elimu ya juu kwa wizara ya fedha iliomba barua ya kujitolea, ishara kwamba hakukuwa na makubaliano rasmi.

Kamati hiyo sasa imeamua kuwaita wawakilishi wa kamati ya mawaziri mbali mbali akiwemo katibu wa elimu ya juu, waziri wa leba na waziri wa fedha kuelezea mustakabali wa serikali na kufafanua hali ya ufadhili wa utekelezaji wa makubaliano ya pamoja ya mwaka 2021 hadi 2025.

Website |  + posts
Share This Article