Mgomo wa wafanyakazi wa shirika la Posta ulioanza tarehe 2 mwezi Novemba mwaka huu wa 2023 umesitishwa, baada ya pande husika kukubaliana kuhusu mchakato wa kurejea kazini.
Wafanyikazi hao waligoma baada ya kukamilika kwa makataa ambayo walikuwa wametoa kwa mwajiri wao kabla ya kuanza mgomo wakidai kulipwa malimbikizi ya mishahara.
Watendakazi hao wa Posta wanadai kutolipwa mishahara tangu mwezi Julai mwaka huu na matozo yao ya lazima nayo hayakuwa yamewasilishwa kwa muda huo.
Kuputia kwa taarifa kwa vyombo vya habari, wizara ya leba na utunzaji wa jamii imetangaza mchakato wa wafanyakazi hao kurejea kazini huku matakwa yao yakishughulikiwa.
Taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano COWU Benson Okwaro kati ya wawakilishi wengine wa wafanyakazi hao, inasema kwamba kwenye mkutano wa Novemba 1, 2023, walikubaliana kusitisha mgomo huo kwa siku 30 kwa masharti yafuatayo;
1. Mishahara ipatiwe kipaumbele pindi shirika hilo litakapopokea malipo kutoka kwa IEBC.
2. Mishahara ya miezi ya Julai, Agosti, Septemba, Oktomba na Novemba iwe imelipwa kikamilifu kufikia Novemba 30, 2023.
3. Usimamizi wa shirika la Posta utafute namna ya kuwasilisha makato ya wafanyakazi katika muda wa siku 21 zijazo.
4. Katibu mkuu na msimamizi wa shirika la Posta wahutubie wafanyakazi kabla ya mgomo kusitishwa.
5. Mgomo urejelewe iwapo masharti hayo hayatatimizwa.
6. Maonevu dhidi ya wafanyakazi kwa kushiriki mgomo yasiwepo.