Mgomo wa wahudumu wa afya kaunti ya Machakos, umeingia siku ya sita leo, huku madaktari hao wakisema hawatalegeza kamba hadi matakwa yao yashughulikiwe.
Mwenyekiti wa chama cha Madaktari na wataalam wa meno(KMPDU) eneo la mashariki mwa nchi Charles Okumu, alisema ugatuzi wa sekta ya afya unapaswa kuhakikisha huduma za afya zinapaswa kupatikana kwa kila mmoja na wahudumu wa afya kupewa motisha.
Akizungumza katika kaunti ya Machakos, Okumu alisema agizo la mahakama linalowataka kurejea kazini, linakiuka haki zao.
Baadhi ya maswala aliyosema wanataka yashughulikiwe ni pamoja na kupandishwa vyeo na kupewa bima ya afya, maswala ambayo wameshinikiza kwa muda wa miaka miwili.
Kulingana na Okumu, baadhi ya madaktari wamehudumu kwa muda wa miaka nane bila kupandivya vyeo.