Mfungwa wa asili ya Kenya apatikana amefariki gerezani Marekani

Marion Bosire
2 Min Read
Billy Chemirir alipofikishwa mahakamani awali

Mfungwa wa asili ya Kenya kwa jina Billy Chemirmir, alipatikana akiwa amekata roho kwenye seli katika gereza la Texas.

Chemirir wa umri wa miaka 50 anasemekana kuawa na mfungwa mwenzake.

Alikuwa anatumikia kifungo cha maisha gerezani kwa makosa ya mauaji ambapo aliua kina mama wakongwe wapatao 22 katika muda wa miaka miwili.

Kisa ambacho kilisababisha akamatwe ni cha mama mmoja wa umri wa miaka 91 mwaka 2018 ambaye aliponea jaribio la mauaji.

Chemirir alitumia mto wa kulalia kujaribu kumuua mama huyo na aliporidhika kwamba amefariki akatoweka na vito vyake vya thamani.

Vifo vya kina mama wengi katika maeneo ya wakongwe kuishi peke yao vilitokea na vito vya thamani kutoweka huku wanafamilia wakiamini walikufa tu kawaida lakini vilipozidi, wengi wakawa na shauku.

Hannah Haney msemaji wa idara ya haki za wafungwa katika jimbo la texas ndiye alitoa taarifa kuhusu kifo cha mkenya huyo lakini hakutaja jina la mfungwa mwenza aliyemuua.

Haya yanajiri wiki mbili tu baada ya jela zote katika jimbo la Texas kufungwa kwa umma baada ya visa vya wafungwa kuuana kukithiri.

Wasimamizi wanaamini madawa ya kulevya ndiyo yalisababisha hali hiyo ndiposa wakaamua kufunga magereza hayo yasifikike na watu kutoka nje wanaoaminika kuwapa wafungwa madawa ya kulevya.

Chemirir alikuwa akifanya kazi kama mhudumu wa nyumbani wa wakongwe nchini Marekani na hivyo ndivyo alikuwa anawafikia na kuwadhuru.

Share This Article