Katibu mkuu wa elimu ya msingi Dkt. Belio Kipsang, amesema hatua ya kuchukua mara mbili karatasi za mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne-KCSE, imezuia udanganyifu.
Katibu huyo alisema mpango huo mpya umeondoa kufunguliwa mapema wa karatasi za mtihani, na hivyo kuepusha udanganyifu.
Akiongea katika shule ya upili ya wasichana ya Naivasha siku ya Ijumaa, Dkt. Kipsang alibainisha kuwa wizara yake imekuwa ikishirikiana na idara ya usalama na ile ya habari ili kupunguza kiwango cha udanganyifu katika mitihani ya mwaka huu.
” Kati ya wasimamizi 11,000 wa vituo vya mitihani, ni saba tu waliopatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani na wamesimamishwa kazi huku uchunguzi ukiendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Kipsang.
Aidha, alisema helikopta kadhaa zimewekwa tayari ili kusaidia katika kuwasilisha mitihani katika vituo vinavyokabiliwa na mafuriko kwa lengo la kuhakikisha watahiniwa wote wanafanya mitihani yao.
Kipsang pia alitangaza kuwa hatua ya kusahihisha mtihani wa kitaifa wa darasa la nane-KCPE imeanza, ili matokeo yatolewe kwa wakati ufaao.
Mwaka huu watahiniwa 903,260 watafanya mtihani wa KCSE hapa nchini.