Mfanyabiashara aliyejiteka nyara punde baada ya harusi yake akamatwa Tanzania

Mkazi huyo wa Kigamboni anatuhumiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi wa kuaminiwa baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutengeneza hisia kwa umma kuwa ametekwa nyara.

Marion Bosire
2 Min Read
Vincent Peter Massawe

Polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam wamesema kwamba walimpata na kumkamata Vincent Peter Massawe maarufu kama Baba Harusi Dicemba 15,2024.

Mkazi huyo wa Kigamboni anatuhumiwa kwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi wa kuaminiwa baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutengeneza hisia kwa umma kuwa ametekwa nyara.

Novemba 19, 2024 Polisi wa Kigamboni walipokea taarifa ya kupotea kwa mfanyabiashara huyo anayedaiwa kutoonekana toka November 18, 2024 baada ya harusi yake na alipotea akitumia gari Toyota Ractis no T 642 EGU ya Sylvester Masawe.

Baadaye ilibainika kwamba aliuza gari hilo badala ya kurudishia mwenyewe baada ya harusi yake November 16, 2024.

Baadaye anadaiwa kwenda kujificha huko Pemba Chakechake Mgogoni kwa mganga wa kienyeji aitwaye Hamis Khalid.

Kamanda wa Polisi wa kanda maalum ya Dar es salaam, Muliro Jumanne amesema Massawe alikiri kutekeleza makosa hayo ambapo anadaiwa kuchukua pesa kutoka kwa watu mbali mbali.

Anaripotiwa kuchukua milioni 55 pesa za Tanzania na gari nambari T 642 EGU aina Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa Sylivester Massawe, milioni 10 kwa udanganyifu kutoka kwa Ramadhani Mkazi wa Magomeni na milioni 15 kutoka kwa Ramadhani Bakari Mkazi wa Temeke.

Massawe alichukua pesa pia kwa udanganyifu kutoka kwa Resma Mbuguni milioni 5, milioni 4 kutoka kwa Asia Mohamed mkazi wa madale, milioni 1.5 kutoka kwa Ngoma mkazi wa Kibaha na milioni 8 kutoka kwa Fauz Suleimani Mussa.

Fauz mkazi wa Tabata ndiye aliuziwa gari ambalo Massawe aliazima siku ya harusi yake, gari nambari T642 aina ya Ractis mali ya Sylivester Massawe.

Uchunguzi kuhusu kesi hiyo unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *