Mexico huenda ikapata Rais wa kwanza wa kike mwakani

Marion Bosire
2 Min Read
Seneta Xóchitl Gálvez na Claudia Sheinbaum

Taifa la Mexico ambalo wengi hulitizamia kuwa linalopendelea wanaume sana huenda likapata Rais wa kwanza wa kike kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Hii ni baada ya chama tawala na muungano wa upinzani kuteua wawaniaji wa kike wa wadhifa huo kwenye uchaguzi utakaoandaliwa Juni 2, 2024.

Chama tawala kiitwacho Morena kimemteua aliyekuwa Meya wa jiji la Mexico Claudia Sheinbaum kuwania urais.

Sheinbaum ni mwanasayansi wa masuala ya tabianchi ambaye aliingilia siasa na anapendelewa kama mrithi na Rais wa sasa Andrés Manuel López Obrador.

Huenda akafaidi kutokana na umaarufu wa Rais Obrador kwenye uchaguzi ujao huku chama cha Morena kikiwa na imani ya kuibuka kidedea.

Seneta Xóchitl Gálvez ambaye ameteuliwa na upande wa upinzani kuwania Urais nchini Mexico hata hivyo anasababisha ujasiri wa chama cha Morena kutiliwa shaka.

Gálvez ni mfanyabiashara ambaye alichaguliwa Seneta mwaka 2018. Hadithi ya maisha yake ilisisimua wengi hasa kuhusu jinsi alilelewa na wazazi wa kitamaduni na akajipigania akasoma hadi chuo kikuu, akaanza biashara na sasa ni mwanasiasa.

Katika muda wa miezi michache tu, ameweza kushawishi vyama vikuu vya upinzani nchini Mexico kumpendekeza kuwania wadhifa wa Urais.

Kina dada hao wawili walipitia mchujo katika vyama vyao ingawaje upande wa upinzani haukukamilisha awamu ya mwisho kwa sababu mpinzani wa Gálvez, Beatriz Paredes alijiondoa.

Mshindani mkuu wa Claudia Sheinbaum katika chama cha Morena Marcelo Ebrard amelaumu chama hicho kwa kumpendelea Claudia.

Anadai kwamba kulikuwa na kasoro katika asilimia 14 ya karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi wa mchujo uliondaliwa ili kupata mwaniaji Urais.

Share This Article