Meghan Markle ambaye alikuwa mwigizaji awali kabla ya kuolewa kwenye familia ya kifalme ya Uingereza amewekeza kwenye kampuni ya bidhaa za nywele iitwayo “Highbrow Hippie hair”.
Mwanzilishi wa kampuni hiyo ni Kadi Lee anayefahamika sana kwa kuhudumia watu maarufu katika masuala ya kupaka nywele rangi.
Markle alikiri kwamba aliwahi kutumia rangi ya nywele awali alipohudhuria hafla ya kuzindua bidhaa mpya za kampuni hiyo huko California.
Kando na kuwa mmoja wa wateja wa Lee, Meghan pia ni mwekezaji wa kampuni hiyo inayotengeneza na kuuza bidhaa za kustawisha nywele.
Lee alimtambua Meghan kwenye hotuba yake akisema kwamba wametoka mbali na wamekua pamoja.
Lee alianzisha jukwaa la taarifa za mitindo ya maisha la Highbrow Hippie na mshirika wake Myka Harris mwaka 2012 na kadri miaka inavyosonga, limegeuka kuwa kampuni ya bidhaa ambayo ina afisi zake huko Venice.
Hata hivyo kiwango cha uwekezaji wa Meghan hakikutajwa huku wakiwa na mipango ya kuunda aina nyingine za bidhaa za kustawisha nywele mwakani.