Usimamizi wa hospitali ya Mediheal umeikosoa Wizara ya Afya kwa kukosa kutoa ripoti rasmi kuhusu operesheni zake za upandikizaji wa figo.
Mwanzilishi wa hospitali hiyo Dkt. Swarup Mishra, akiwa ameandamana na wakili wake Katwa Kigen, amepuuzilia mbali madai ya ulanguzi wa viungo vya mwili, na kudokeza kuwa hospitali hiyo bado haijapokea matokeo ya uchunguzi uliotekelezwa na kamati huru ya uchunguzi kuhusu upandikizaji wa viungo vya mwili.
Wakati huo huo, hospitali hiyo imekanusha madai kwenye mitandao ya kijamii zinazodai hospitali hiyo haikutoa stakabadhi za kutosha, ikisema iliwasilisha rekodi zote zikiwemo taarifa za upandikizaji 476 ilizofanya tangu mwaka 2008.
Akiwahutubia wanahabari leo Jumanne, Dkt. Mishra alitaja madai hayo kuwa ya kupotosha na yaliyolenga kuiharibia sifa hospitali hiyo.
Kulingana na Dkt. Mishra, hospitali hiyo haijawahi kuhusika katika kisa chochote cha ulanguzi wa figo, akidokeza kuwa huwa wanatekeleza upandikizaji wa figo kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
Waziri wa Afya Aden Duale alibuni kamati huru ya kuchunguza madai ya ulanguzi wa viungo vya mwili kwenye hospitali hiyo na kupendekeza mashtaka dhidi ya mwanzilishi na mwenyekiti wake Dkt. Swarup Mishra.