Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakango afikishwa mahakamani

Martin Mwanje
2 Min Read

Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakango leo Jumanne alifikishwa katika mahakama moja ya Mombasa akikabiliwa na mashtaka manne yanayohusiana na udanganyifu. 

Mashtaka hayo yaliwasilishwa na Claudia Mueni Mutungi dhidi yake na watu wengine 10.

Nyakango alikanusha mashtaka dhidi yake na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni mbili au laki tano pesa taslimu.

Kesi dhidi yake sasa itasikizwa Disemba 13.

Nyakango pamoja na watu wengine wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukula njama ya kufanya ulaghai kinyume cha sehemu ya 317 ya kanuni ya adhabu.

Anatuhumiwa kwa kumlaghai Mueni shilingi milioni 29 kati ya Novemba 1, 2019 na Mei 1, 2020 kwa kusingizia kuendesha chama cha ushirika na mikopo kwa jina FEB.

Anakabiliwa na mashtaka hayo kwa pamoja na Jackson Ngure Wanjau, Susan Kendi, James Makena Wanyagi, John Muchira Kithaka, Jane Karuu Ndanyi na Muthoni Elphas, kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Jacinta Nyamosi.

Wengine wanaokabiliwa na mashtaka ni Joan Chumo, Mercy Ndura Mukora, Gregory Mwangangi Mailu na Michael Kipkurui.

“Kwa hivyo, tunaelekeza kwamba washukiwa hawa wote waliotajwa washtakiwe pamoja kwa mashtaka yafuatayo ambayo ni kukula njama ya kufanya ulaghai kinyume cha sehemu ya 317 ya kanuni ya adhabu, kuendesha chama cha akiba na mikopo bila leseni kinyume cha sehemu ya 24 ikisomwa pamoja na sehemu ya 66 ya sheria ya vyama vya akiba na mikopo, kughushi na kutoa waraka wa uongo kinyume cha sehemu ya 353 ya kanuni ya adhabu,” inaongeza taarifa hiyo.

 

 

Share This Article