Mchungaji Dorcas Rigathi kuanzisha vituo vya kuwarekebisha tabia waraibu wa mihadarati

Marion Bosire
2 Min Read

Mkewe Naibu Rais mchungaji Dorcas Rigathi ana mpango wa kuzindua vituo vya kutibu na kurekebisha tabia waraibu wa pombe na mihadarati nchini. Mchungaji huyo alialikwa nchini Israel kwa ziara ya kujifahamisha kuhusu miundo faafu ya vituo kama hivyo ambavyo anapanga kuanzisha humu nchini.

Alisema mpango huo unaangazia kikamilifu mchakato wa kuwabadili tabia, kuwafanya upya na kuwatibu waathiriwa. Waathiriwa hutolewa kwenye mazingira yao ya kawaida na kupelekwa kwenye vituo hivyo vinavyorejelewa kama vijiji, ambavyo huwafanya wahisi kama wako nyumbani kando na vituo ambavyo vina muundo kama wa shule ya bweni.

Katika vituo hivyo, waathiriwa hupatiwa uhuru kipindi chote cha maytibabu ambacho huwa kati ya miezi mitano na minane.

Mkewe Naibu Rais ana imani kwamba matibabu kama hayo yakitekelezwa nchini yatasaidia sana kwani alivyoona nchini Israel, waathiriwa huondoka wakiwa wanaweza kujisimamia kikamilifu.

Alialikwa na kundi la Well-Being International: Global Advisory Group ambalo limeahidi kutoa usaidizi kwake anapopanga kuanzisha vijiji kama hivyo nchini.

Kwa sasa vijana wapatao 120 kutoka sehemu mbali mbali za nchi wanaendelea kupokea huduma ya kuwarekebisha tabia katika kituo cha Timau na vingine kote nchini, chini ya mpango aliouanzisha mkewe naibu rais.

Mchungaji Dorcas alizuru kijiji cha KFAR IZUN jina linalomaanisha “Kijiji cha usawa” na kijiji cha YEMIN ORDE nchini Israel vituo ambavyo vimesaidia vijana wengi ambao pia walipata ujuzi kabla ya kurejeshwa katika jamii.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *