Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya soka Harambee Stars Collins Okoth Ougo almaarufu Gatusso, amefikishwa katika mahakama ya Milimani akikabiliwa na mashtaka ya mauaji.
Okoth ambaye pia alichezea timu ya Gor Mahia na mshtakiwa mwenza Sylvia Aoko Odhiambo siku ya Jumanne, walifikishwa mbele ya Jaji Alexander Muteti, wakidaiwa kumuua mtoto wa umri wa miaka mitatu Pamela Atieno almaarufu Scovian Maya katika mtaa wa Lucky Summer jijini Nairobi.
Mahakama ilifahamishwa kuwa Okoth pamoja na mshirika wake, walivunja nyumba ya wazazi wa mtoto huyo katika mtaa wa Lucky Summer, wakati wazazi wake hawakuwepo na kutekeleza mauaji hayo.
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana umetupwa karibu na nyumbani kwao.
Mahakama iliagiza washukiwa hao wawili wawasilishwe mahakamani Julai 30, 2024 kujibu mashtaka hayo, baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kiakili.
Okoth atazuiliwa katika gereza la Industrial Area huku mshatkiwa mwenza akizuiliwa katika gereza la wanawake la Lang’ata.