Mabingwa mara mbili wa Afrika Algeria walinusurika kichapo baada ya kutoka sare ya bao 1 kwa moja dhidi ya Angola Jumatatu usiku.
Mechi hiyo ya ufunguzi ya kundi D mjini Bouke Ivory Coast katika kipute cha AFCON ilishuhudia Baghdad Bounedjah, akipachika bao la kwanza kwa Foxes ya Algeria walioongoza kufikia mapumziko.
Palancas Negras ya Angola ukipenda swara walirejea kwa vishindo kunako kipindi cha pili , na kufanya mashambulizi yaliyozaa penati baada ya Mabululu kuangushwa na Nabil Bentaleb.
Mabululu aliunganisha penati hiyo na kuwanyanyua mashabiki wa swara hao kutoka Luanda hadi Abidjan.
Hadi kipenga cha mwisho Algeria na Angola waligawana alama moja.
Awali katika mechi ya kundi C Guinea na Cameroon waliambulia sare ya bao moja.