Mbunge wa Wanawake wa eneo bunge la Kampala, Shamim Malende juzi Jumatano alisafirishwa kwa ndege hadi nchini Kenya ili kupokea matibabu maalum katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.
Kulingana na gazeti la Monitor linalochapishwa nchini Uganda, hatua hiyo ilifuatia ushauri wa daktari baada ya kudorora kwa hali ya afya ya mbunge huyo.
Mbunge huyo anasema chanzo cha matatizo yake ya kiafya ni mafarakano yaliyotokea bungeni mwezi Novemba mwaka jana wakati wa kupitishwa kwa marekebisho ya Mswada wa Taifa wa Kahawa.
Anasema alitendewa vibaya wakati wa machafuko hayo na kutia kidonda kwa majeraha yaliyotokana na upasuaji wa awali aliofanyiwa mnamo mwaka 2022, hali anayosema imefanya majeraha hayo kukawia kupona.
“Nilitendewa vibaya wakati wa vurugu zilizotokea wakati wa usomaji wa Mswada wa Kahawa,” mbunge huyo alinukuliwa akisema.
Tangu kutokea kwa vurugu hizo, amekuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Nsambya.
Hata hivyo, madaktari hospitalini hapo walimshauri kutafuta matibabu maalum katika hospitali ya Aga Khan nchini Kenya alikofanyiwa upasuaji awali.