Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing Jumanne alihojiwa kwa saa sita na polisi katika Kaunti ya Pokot Magharibi kuhusu matamshi ya uchochezi yaliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Wakili wa Pkosing, Jackson Kimani, hata hivyo, alimtetea mteja wake akidai kuwa ujumbe huo haukusudiwa kuchochea bali kueleza wasiwasi wake kama mwakilishi wa wananchi.
Pkosing alisema hana hatia akiongeza kuwa alinuia kuangazia maswala muhimu yanayoathiri watu kwenye mpaka wa Pokot Magharibi na Kaunti ya Turkana.
Afisa wa Upelelezi wa Jinai wa Kaunti ya Pokot Magharibi (CCIO) George Mutonya, hata hivyo, aliona kuwa mbunge huyo alihojiwa kuhusiana na wasiwasi kwamba maneno yaliyotumwa kwenye ukurasa wake wa Facebook yanaweza kusababisha mzozo kati ya Wapokot na jamii jirani.
Mbunge huyo alielezea kusikitishwa kwake na hatua za vikosi vya ulinzi nchini KDF, akivishutumu kwa mauaji ya watu na zaidi ya ng’ombe 100. Alidokeza kuwa maganda ya risasi yaliyopatikana na ambayo yanaaminika kuwa ya KDF, yaliwasilishwa katika kituo cha polisi cha Kapenguria kwa uchunguzi.