Mbunge alaumu TSC kwa kutoshughulikia vyema masuala ya walimu

Marion Bosire
1 Min Read

Mbunge wa eneo la Mbeere Kaskazini Geoffrey Ruku amelalamikia jinsi TSC inashughulikia walimu na sasa anapendekeza mabadiliko katika tume hiyo ili kuhakikisha masuala ya walimu yanapatiwa kipaumbele.

Akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya mwalimu Lawrence Njuki, Rúkú alisema kwamba usimamizi wa tume ya TSC na mashirika mengine ya walimu yamejaa ufisadi.

Kulingana naye, hatua ya kuhamisha walimu mbali na nyumbani almaarufu “delocalization” kumesababishia wengi matatizo na hata kusababisha familia nyingi kuvunjika.

Anasema wito uliotolewa na wabunge kwa TSC kubatilisha uhamisho huo haujazaa matunda.

Mbunge huyo alisema marehemu Lawrence alikuwa amelalamika kwa muda mrefu kuhusu kuhamishwa na alitaka kurejeshwa karibu na nyumbani ili atunzwe na familia lakini hakufanikiwa.

Ruku amesema kwamba bunge halitaunga mkono afisa yeyote wa serikali anayezembea kazini kwa gharama ya maisha ya wakenya. Aliongeza kwamba wabunge watawatimua maafisa wote wasiowajibika kazini na ambao wanahujumu Rais.

Share This Article