Siku chache baada ya taarifa za Mbosso kuruhusiwa kuondoka kwenye kampuni ya Wasafi, msanii huyo amechukua hatua ya kufuta machapisho yote ya awali kwenye akaunti yake ya Instagram.
Hata hivyo msanii huyo amedumisha kwenye wasifu wake kwamba yeye amesajiliwa na kampuni ya kusimamia wanamuziki ya WCB inayomilikiwa na Diamond Platnumz.
Wadadisi wanahisi kwamba Mbosso anajiandaa kufungua ukurasa mpya nje ya kampuni ya Wasafi kama msanii huru.
Mange Kimambi anasema kwamba wasanii hutaka kuondoka kwenye kampuni hiyo kwani “hawapati matunda ya kazi zao, wanapiga kazi kubwa, wanakuwa maarufu nchi nzima ila hakuna pesa ya maana wanayopata.”
Kulingana naye faida kubwa huwa inaenda kwa kampuni ndio maana wanaona bora watoke wakajitafutie hata kama ni kidogo ila angalau ni chake na hatumiki tena kutajirisha mtu.
Inasubiriwa kuona jinsi Mbosso ambaye jina lake halisi ni Mbwana Yusuf Kilungi ataanza safari yake kama mwanamuziki huru.
Wasanii wengine ambao waliondoka WCB ni pamoja na Rich Mavoko ambaye hakukaa huko sana, Rayvanny ambaye alianzisha kampuni yake ya Next Level Music na Harmonize ambaye alianzisha pia kampuni yake kwa jina Konde Music World Wide.
Harmonize na Rayvanny walikwazana kidogo na WCB kuhusu ada ambazo walistahili kulipa kabla ya kuruhusiwa kuondoka lakini Mbosso ameruhusiwa kuondoka bila malipo yoyote.
Inaripotiwa kwamba WCB inapanga kusajili wasanii 9 mwaka huu wa 2025.