Mbivu na mbichi ya ‘Baba’ kubainika leo AU

Dismas Otuke
2 Min Read
Raila Odinga - Mgombea wa uenyekiti wa AUC

Baada ya kampeni moto moto na subira ya muda mrefu, hatimaye mbivu na mbichi ya Raila Odinga itabainika leo wakati marais na viongozi 49 watapiga kura za kumchagua mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.

Uchaguzi huo utaandaliwa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika – AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Raila anamenyana na wapinzani wengine wawili, Richard Randriamandrato wa Madagascar na Mahamoud Youssouf kutoka Djibouti.

Mataifa ya Burkina Faso, Mali, Guinea, Niger, Gabon na Sudan hayatapiga kura baada ya kupigwa marufuku kutokana na mapinduzi ya serikali na wanajeshi.

Ili kutangazwa mshindi, Raila anahitaji kupata kura 33 katika raundi ya kwanza ya upigaji kura.

Endapo hakuna mwaniaji atakayepata ushindi katika raundi ya kwanza, upigaji kura utaingia raundi ya pili, ambapo mwaniaji wa mwisho katika raundi ya kwanza ataondolewa kwenye debe.

Raundi ya tatu ya upigaji kura itahitajika ikiwa hakutakuwa na mshindi atakayepata thuluthi mbili ya kura kwenye raundi ya pili; mgombeaji atakayemaliza wa pili akiondolewa.

Mwaniaji atakayeongoza raundi ya pili pekee atashirikishwa katika raundi ya tatu ya upigaji kura.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ina jumla ya kura 16, huku mataifa mengi yakitarajiwa kumuunga mkono mgombeaji wa Madagascar.

Raila kwa upande wake anatarajiwa kupata uungwaji mkubwa kutoka kwa mataifa manane ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), huku Youssouf akilenga kupata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wa IGAD.

Kando na miungano ya kiuchumi, huenda mataifa hayo 49 yakapiga kura kwa kuzingatia ushirikiano wa kidiplomasia na nchi zilizo na wawaniaji.

Mwenyekiti mpya atamrithi Moussa Faki wa Chad, ambaye amehudumu tangu mwaka 2017.

Raila amezuru takriban mataifa yote 49 ya Afrika yatakayopiga kura katika juhudi za kutafuta uungwaji mkono, zoezi ambalo limepigwa jeki na serikali ya Kenya.

Website |  + posts
Share This Article