Mazungumzo ya Upatanisho: Timu za Kenya Kwanza na Azimio zakutana

Martin Mwanje
2 Min Read

Timu za utawala wa Kenya Kwanza na muungano wa upinzani wa Azimio zilikutana Bomas of Kenya leo Jumatatu na kukubaliana juu ya kuundwa rasmi kwa timu za kiufundi za pande zote ambazo zitafanya kazi na timu za mazungumzo.

Timu ya kiufundi ya Kenya Kwanza inawajumuisha wakili Dkt. Muthomi Thiankolu. Dkt. Linda Musumba, Dkt. Duncan Ojwang ambaye ni mhadhiri wa sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi na Nick Biketi.

Kwa upande mwingine, wanachama wa timu ya kiufundi ya muungano wa Azimio inajumuisha mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni, Prof. Adams Oloo ambaye pia ni mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Zein Abubakar na Lynn Ngugi.

Timu hizo mbili za kiufundi zimetakiwa kuunda ajenda ya mazungumzo hayo itakayozingatiwa na kamati ya mazungumzo na vilevile zimetakiwa kupitia upya makubaliano ya mpangokazi wa mazungumzo ya pande mbili ili kujumuisha maazimio ya timu za mazungumzo.

Aidha, timu za Kenya Kwanza na Azimio zilikubaliana kwamba uongozi wa bunge la kitaifa na seneti uandae hoja itakayobuni timu ya majadiliano kisheria.

Bunge la kitaifa linatarajiwa kuandaa hoja hiyo wiki hii huku uongozi wa bunge la seneti ukitarajiwa kuitisha kikao maalum kuandaa hoja hiyo kwani kwa sasa, bunge hilo liko mapumzikoni.

Kulingana na taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa ambaye pia anaongoza timu ya Kenya Kwanza katika mazungumzo hayo Kimani Ichung’wah na Kalonzo Musyoka anayeongoza Wanaazimio, timu hizo mbili zitakutana tena Jumatatu wiki ijayo.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *