Muguka: Magavana wa Pwani wakataa mwaliko wa Linturi

Kevin Karunjira
2 Min Read
Gavana wa kaunti kaunti ya Kilifi Gideon Mung'aro

Magavana wa kaunti za Pwani wamekataa mwaliko wa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi wa kukutana ili kuangazia suala tata la zao la Muguka. 

Walifikia uamuzi huo baada ya kukutana chini ya Jumuiya ya Kaunti za Pwani inayozileta pamoja kaunti za Mombasa, Kilifi, Taita Taveta, Kwale na Lamu.

Katika taarifa iliyotiwa saini na Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro, Magavana hao wanasema Waziri Linturi hawezi kuongoza mazungumzo ya kutafuta mwafaka kuhusiana na zao hilo kwani tayari ameweka wazi msimamo wake.

“Kama Waziri wa Kilimo, umeelezea wazi juu ya misimamo ya kikatiba na kisheria iliyochukuliwa na Magavana wa kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita ya kupiga marufuku Muguka. Kulingana na taarifa zako za Mei 29, 2024, msimamo wa Wizara yako ni ule wa kulinda chumi za kaunti zinazozalisha zao hilo,” walisema Magavana hao katika taarifa.

“Kwa kuzingatia Jumuiya ya Kaunti za Pwani kuwa eneo linalotumia zao hilo na iliyo na maslahi ya usalama wa kijamii, kiuchumi na afya, kwa heshima, tunahitimisha kuwa huwezi kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote kuhusiana na suala hilo.”

Magavana hao sasa wanamtaka Rais William Ruto kuongoza mazungumzo ya kutafuta mwafaka juu ya suala hilo ikizingatiwa kwamba siku chache zilizopita, alifanya mikutano na serikali za kaunti zinazozalisha Muguka na uongozi wa Mlima Kenya na kutoa maelekezo kuhusiana na suala hilo.

Zao la Muguka lilikuwa limepigwa marufuku na kaunti za Mombasa, Kilifi na Taita Taveta kabla ya mahakama kubatilisha uamuzi huo hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikilizwe na kuamuliwa.

Gavana wa Embu Cecily Mbarire, kunakozalishwa zao hilo kwa wingi, amekuwa mstari wa mbele kupinga hatua ya kaunti za Pwani kupiga marufuku matumizi ya Muguka kwa madai kuwa zao linasababisha madhara ya kiafya na mengineyo kwa wakazi wengi wa kaunti hizo.

Zao hilo linasemekana kuziletea kaunti zinazolizalisha mamilioni ya pesa.

 

 

 

Share This Article