Mawaziri wapya waliingia katika ofizi zao kwa vishindo wakiwa tayari kulitumikia taifa yamkini kwa udi a uvumba, saa chache baada ya kuapishwa katika Ikulu ya Nairobi.
Hafla ya uapishaji wa mawaziri hao 19 iliongozwa na Rais William Ruto na kuhudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na maafisa wengine wa ngazi za juu serikali.
Punde baada ya kuapishwa, mawaziri hao walifululiza moja kwa moja hadi ofizi zao mpya na kukaribishwa na makatibu na maafisa wengine wa ngazi za juu wizarani.
Katika Wizara ya Fedha, Waziri John Mbadi alilakiwa na Makatibu Dkt. Chris Kiptoo na James Muhatia.
Katika Wizara ya Vyama vya Ushirika, Waziri Wycliffe Oparanya alilakiwa na Katibu Susan Mang’eni na maafisa wengine katika wizara hiyo.
Mawaziri wengine walioapishwa leo Jumanne ni Prof. Kithure Kindiki (Usalama wa Taifa) Debra Barasa (Afya), Alice Wahome (Ardhi), Julius Ogamba (Elimu), Soipan Tuya (Ulinzi), Andrew Karanja (Kilimo), Aden Duale (Mazingira), Eric Muuga (Maji na Usafi), Davis Chirchir (Barabara na Uchukuzi) na Margaret Ndung’u (Habari, Mwasiliano na Uchumi wa Digitali).
Wengine ni Salim Mvurya (Biashara), Rebecca Miano (Utalii), Opiyo Wandayi (Nishati), Kipchumba Murkomen (Michezo), Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Baharini), Alfred Mutua (Leba) na Justin Muturi (Utumishi wa Umma).
Kamati ya bunge kuhusu uteuzi iliwaidhinisha mawaziri hao wateule 19 huku ikikatalia mbali uteuzi wa Stella Lang’at kuwa Waziri wa Jinsia kwa misingi kwamba hakuonyesha kuwa na ufahamu wa masuala katika wizara hiyo wakati wa usaili wake.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kwa mawaziri hao katika Ikulu, Rais Ruto aliwataka Wakenya kuwapa fursa ya kuwatumikia akisema ana imani watabadilisha hali ya nchi na kuifanya kuwa bora zaidi.