Mawasiliano na utekelezaji duni vyasemekana kuhujumu CBC

Spika Wetangula alizungumza hayo alipokutana na wanafunzi wa shahada ya uzamifu katika masuala ya uongozi katika chuo cha USIU

Marion Bosire
2 Min Read
Moses Wetangula, Spika wa Bunge la Taifa

Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula amesema kwamba mawasiliano duni pamoja na utekelezaji duni ndivyo vitu ambavyo vinahujumu mtaala wa umilisi nchini yaani CBC.

Akizungumza alipokutana na ujumbe wa wanaosomea shahada ya uzamifu katika uongozi katika chuo kikuu cha USIU afisini kwake, Wetang’ula, alihimiza mpango makhsusi wa utekelezaji wa mtaala huo.

Mkutano huo uliangazia masuala muhimu yanayoathiri sekta ya elimu nchini Kenya, ajenda ya nyumba za gharama nafuu na hatari za mianya iliyopo kwenye tume ya uchaguzi na mipaka IEBC.

Profesa Timothy Oketch anayesimamia taasisi ya Chandaria ya masomo ya biashara aliyeongoza ujumbe huo aliangazia tatizo la wahitimu kutoweza kuajirika nchini huku kukiwa na vyuo vikuu zaidi ya 70.

Alisema madarasa yaliyofurika wanafunzi na ukosefu wa usawa kati ya mafunzo na mahitaji ya soko la ajira ni masuala muhimu yanayofaa kuangaziwa.

“Sera zipo lakini utekelezaji haupo.” alisema Oketch huku akihimiza uwekezaji zaidi katika ujumuishaji, kuboresha mabadiliko ya kidijitali na kuimarishwa kwa vyuo anuwai na vyuo vikuu.

Anahisi kwamba taasisi hizo zikiboreshwa, zitaandaa vijana kwa ajira za siku zijazo.

“Kilimo kinaendesha asilimia 60 ya uchumi wetu lakini ujuzi wa biashara, kazi za dijitali na akili mnemba ndio una ushindani wa kiwango cha juu.” alisema Oketch.

Wetang’ula anasisitiza umuhimu wa kuhakikisha elimu inayotolewa inaambatana na mahitaji ya soko la ajira nchini.
Anataka pia dhana kwamba elimu inahakikishia mtu ajira itupiliwe mbali.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *