Mawakili bandia wakamatwa Kasarani, Nairobi

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa polisi walivamia nyumba moja ya makazi mtaani Kasarani kaunti ya Nairobi na kukamata wanawake wawili ambao wamekuwa wakiendesha afisi ya uwakili kinyume cha sheria.

Walikamatwa na maafisa wa upelelezi na viongozi wa chama cha mawakili nchini LSK, wakiendeleza kazi zao kwenye jengo la makazi karibu na kituo cha polisi cha Kasarani.

Washukiwa walipelekwa kwenye kituo hicho cha polisi na maafisa wa upelelezi wa jinai DCI na wanasubiri kufikishwa mahakamani wakati wowote kwa makosa ya kujisingizia kuwa mawakili na kugushi stakabadhi za kisheria.

Stephen Mbugua wa kundi la hatua za haraka la chama cha LSK aliyeongoza oparesheni hiyo akiwa na wenzake Teresia Wavinya na Gloria Kimani, alisema inaonekana kwamba mawakili bandia sasa wamebadili mtindo na wanatumia nyumba za makazi kama afisi ambapo wanaweza kulenga wasiojua.

Mbugua alisema kwamba stakabadhi za kuthibitisha ubadilishanaji zilipatikana kutoka kwa wawili hao zikiwemo za kubadilishana mali na wasia huku akionya wananchi wawe macho wasiangukie mikono ya wahalifu hao.

Wavinya alionya wenzao katika taaluma ya uwakili dhidi ya kujihusisha na watu ambao hawajahitimu katika taaluma hiyo kwani wanajiweka katika hatari ya kuchukuliwa hatua ikiwemo ya kuondolewa kwenye sajili ya mawakili.

Share This Article