Wabunge wawili katika kaunti ya Laikipia wametoa wito wa kuharakishwa kwa uchunguzi kuhusu mauaji ya Agnes Wanjiru yaliyotokea miaka 13 iliyopita.
Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti hiyo Jane Kagiri na mbunge wa Laikipia Kaskazini Sarah Korere wanasema kuharakishwa kwa uchunguzi huo kutahakikisha familia ya marehemu inapata haki.
Akitaka Wanjiru aliyedaiwa kuuawa mjini Nanyuki na mwanajeshi Mwingereza kutendewa haki, Korere alisema Kenya imeshuhudia ongezeko la wanawake katika miaka ya hivi karibuni.
Aidha, mbunge huyo alitaka watu walioteseka kutokana na mafunzo ya jeshi la Uingereza katika eneo bunge lake kutendewa haki.
Wawili hao walizungumza katika eneo la Survey katika wadi ya Sosin, eneo bunge la Laikipia Kaskazini wakati wa uzinduzi wa mpango wa uboreshaji wa visima vya maji ulioongozwa na Katibu wa Unyunyiziaji Mashamba Maji Ephantus Kimotho.
Kimotho alisema visima vitano vya maji vitaboreshwa huko Laikipia chini ya Mpango Uliohuishwa wa Unyunyiziaji Mashamba Maji katika maeneo kame nchini na kuongeza kuwa kaya 100 zitanufaika kutokana na maji yatakayotoka kwenye visima hivyo vilivyoboreshwa.
Wakati huo, Korere na Kagiri walitetea uamuzi wao wa kusalia katika serikali ya Kenya kwanza wakisema hiyo ndio njia pekee ya kuvutia maendeleo yanayfadhilwa na serikali.
Korere alisema uboreshaji wa visima vitano unaofanywa na Mamlaka ya Taifa ya Unyunyiziaji Mashamba Maji utaboresha uzalishaji chakula na kipato cha maisha ya watu.