Rais William Ruto amependekeza kwamba matumizi ya fedha za umma yapunguzwe pakubwa katika afisi kuu za nchi kufuatia kutupiliwa mbali kwa mswada wa fedha wa mwaka 2024.
Akihutubia taifa kutoka ikulu ya Nairobi, Rais alielezea kwamba kufuatia kuondolewa kwa mswada huo ambao ungesaidia kukusanya mapato zaidi ya kutosheleza bajeti ya taifa, ni lazima matumizi yapunguzwe.
Afisi ya Rais ni mojawapo ya asasi alizozitaja Rais Ruto ambazo zitapunguza matumizi yake ambapo fedha za kuendesha afisi za serikali kuu zitapunguzwa, fedha za usafiri, za makaribisho ya wageni,za kununua magari, za ukarabati na matumizi mengine zitapunguzwa.
Kiongozi wa nchi alipendekeza pia kwamba asasi nyingine za serikali kama bunge, idara ya mahakama na serikali za kaunti zishirikiane na wizara ya fedha kupunguza matumizi ya fedha.
Ruto amechukua hatua hii kufuatia shinikizo za wakenya kupitia maandamano katika sehemu mbli mbali za nchi. Wananchi wanahisi kwamba tayari wanatozwa ushuru wa kiwango cha juu na nyongeza iliyokuwa imependekezwa ya ushuru ingewaumiza zaidi.
Hata baada ya maalamiko hayo bunge lilipitisha mswada huo baada ya marekebisho fulani na hatua iliyokuwa imebaki ni ya Rais kuutia saini kuwa sheria lakini amekataa na amewataka wabunge kuutupilia mbali.
Viongozi kadhaa wakiwemo wa kidini awali walikuwa wametoa wito kwa Rais kuutupilia mbali mswada huo kama njia ya kuhakikisha utulivu nchini.