Matayarisho ya maadhimisho ya 14 ya Siku ya Mashujaa yameanza kwa vishindo.
Siku ya Mashujaa huadhimishwa nchini kila Oktoba 20 na mwaka huu sherehe za siku hiyo zitaandaliwa katika kaunti ya Kericho.
Katika uwanja wa michezo wa Kericho, shughuli za ukarabati zimepamba moto huku serikali ikisema iko makini kuongeza idadi ya watu wanaoweza kutoshea uwanjani hapo hadi 10,000.
Katibu katika Wizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo leo Alhamisi aliwaongoza maafisa wengine wakuu wa serikali kutembelea uwanja huo.
Alisema ukarabati huo utajumuisha ujenzi wa sehemu zingine tatu za kukalia ili kuwasheheni watu wengi zaidi.
Kulingana na Dkt. Omollo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati inayosimamia sherehe za kitaifa, kila ya maeneo mawiili yanayoungana na jukwaa kuu yatawekwa viti 1,000 zaidi na vingine 1,000 kuwekwa katika maeneo mengine ya kukalia.
Aliongeza kuwa uwanja huo utawekewa huduma muhimu kama vile umeme, maji na mfumo wa kupitisha maji taka.
Aidha miradi ya miundombinu imepangwa kutekelezwa katika kaunti ya Kericho kama moja ya manufaa yanayokuja kutokana na kaunti kuwa mwenyeji wa sherehe za kitaifa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa barabara.
Katibu huyo alidokeza kuwa maudhui ya sherehe za mwaka huu yatakuwa upatikanaji wa afya kwa wote ambayo ni moja ya nguzo ambazo serikali imependekeza malengo ya maono ya mwaka wa 20230.