Mataifa ya Afrika ya kati yaunga mkono ECOWAS

Tom Mathinji
2 Min Read

Jumuiya ya kanda ya Afrika ya Kati ECCAS, imeunga mkono juhudi za wenzao wa Afrika Magharibi, ECOWAS katika kurejesha utaratibu wa kikatiba nchini Niger.

Hayo ni Kwa mujibu wa Rais wa Nigeria ambaye pia ni Mwenyekiti wa ECOWAS Bola Tinubu, baada ya ziara ya mjumbe maalumu wa Rais wa Gabon na Mwenyekiti wa ECCAS, Ali Bongo Ondimba kwenye ikulu ya Abuja, mji mkuu wa Nigeria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Gabon, Hermann Immongault, alisema Rais Bongo “alilaani vikali” mapinduzi ya Niger na kuunga mkono hatua zote za ECOWAS zilizochukuliwa kurejesha demokrasia nchini Niger.

ECOWAS ilikuwa imetoa vikwazo kadhaa ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa mpaka nchini Niger, ambapo mapinduzi ya kijeshi yalimwondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26.

Jumuiya ya kikanda ilisema itapeleka kikosi cha ECOWAS nchini Niger ili kurejesha utulivu wa kikatiba kufuatia kumalizika kwa makataa ambayo yalitolewa kwa viongozi wa mapinduzi kumrejesha madarakani Rais aliyeng’olewa madarakani.

Hata hivyo haikutoa muda wa matumizi ya nguvu ambayo ilisema ni “chaguo la mwisho” iwapo chaguzi zote za kidiplomasia na kisiasa zitashindwa.

Wakuu wa ulinzi kutoka eneo hilo wanakutana mjini Accra siku ya Alhamisi na Ijumaa ili kujadili uwezekano wa suluhu la mgogoro wa Niger.

Mapinduzi ya kijeshi yamevutia hisia za kimataifa huku serikali nyingi za kigeni zikitoa wito wa kutatuliwa mgogoro huo kwa amani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken Jumanne alisema Marekani inaamini bado kuna “nafasi ya diplomasia” katika kufanikisha kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *