Mashirika yasiyo ya serikali kuimarisha huduma za afya Mandera

Dismas Otuke
2 Min Read

Mashirika yasiyo ya kiserikali yameshirikiana na serikali ya kaunti ya Mandera kuboresha viwango vya afya katika kaunti hiyo.

Shirika linalofahamika kama Action Against Hunger limeshiarikiana na serikali ya kaunti ya Mandera kuboresha mpango huo.

Mchango huo unaojumuisha vifaa mbalimbali vya matibabu, umetengewa vituo 18 vya huduma za afya katika kaunti ndogo za Mandera Kaskazini, Mandera Kusini, Mandera Magharibi na Banisa.

Mohammed Ali Omar, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kaunti ya Mandera kuhusu Afya, aliusifia mpango huo na kusisitiza uwezo wake wa kuimarisha viwango vya afya kwa makundi yaliyo katika hatari.

“Tumetoa viifaa muhimu kama vile mizani ya kupimia uzito wa mama na mtoto, vitanda vya watoto wachanga, vipimajoto, mashine za shinikizo la damu na taa za uchunguzi hulenga kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, hasa vijijini na vitongojini ,” alisema.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo kwenye hospitali ya rufaa ya kaunti ya Mandera, mratibu wa shirika la Action Against Hunger, Ali Bashir, alikariri kuwa lengo kuu la mchango kuimarisha huduma ya afya ya jamii.

Mvua iliyonyesha majuzi imeleta changamoto kubwa kwa mfumo wa afya wa kaunti ya Mandera, haswa kwa kuathiri vituo 23 vya afya huko Mandera Magharibi, Kotulo, Mandera Mashariki na Arabia.

Mchango huu unasimama kama njia muhimu ya kuokoa maisha kwa kutoa msaada muhimu, ili kupunguza mzigo kwenye huduma za afya katika maeneo haya yaliyoathiriwa na mvua.

Share This Article