Mashahidi zaidi ya 200 kutoa ushahidi dhidi ya Mandago na wenzake

Martin Mwanje
1 Min Read

Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma inanuia kutumia mashahidi 202 katika kesi ya sakata ya shilingi bilioni 1.1, pesa zilizokusudiwa kufadhili masomo ya wanafunzi kutoka kaunti ya Uasin Gishu katika nchi za Ufini na Canada.

Seneta wa kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago pamoja na washukiwa wengine wawili wa sakata hiyo Joshua Lelei na Meshack Rono wamefika mahakamani leo Jumatatu kesi hiyo ilipotajwa.

Watatu hao wanadaiwa kuhusika katika matumizi mabaya na wizi wa pesa hizo zilizochangwa na familia za wanafunzi waliotarajia kunufaika na mpango huo.

Upande wa mashtaka pia umedokeza utatumia stakabadhi zingine kama ushahidi ambazo kufikia leo hazikuwa zimefikia mawakili wa washukiwa.

Mawakili wa washukiwa hao wameomba siku 60 ili kujifahamisha na stakabadhi hizo.

Hakimu Peter Ndege ameelekeza kuwa kesi hiyo itajwe Januari 14 mwaka ujao.

Mandago na washukiwa wenzake wanakabiliwa na mashtaka kumi yakiwemo kupanga njama na kuiba fedha hizo, matumizi mabaya ya ofisi zao na kughushi stakabadhi walizotumia kutoa fedha hizo kwenye benki.

Share This Article