Bunge la Senate Alhamisi usiku lilimwondoa afisini Rigathi Gachagua, baada ya kumpata na makosa 5 kati ya 11 yaliyomkabili.
Gachagua ambaye anakuwa Naibu Rais wa kwanza kuondolewa mamlakani hapa nchini chini ya katiba ya mwaka 2010, alikuwa akipokea matibabu katika hospitali moja Nairobi mchakato huo ulipokuwa ukiendelea.
Maseneta hao walipigia kura kila kosa, na hivi ndivyo walivyopiga:
Katika kosa la kwanza ambalo ni ukiukaji wa vifingu 10 (2)(a), (b) and (c); 27 (4), 73 (1)(a) and (2)(b); 75 (1)(c) na 129 (2) vya katiba, Maseneta 54 waliunga mkono, 13 wakipinga.
Katika kosa la pili, ambapo alishtakiwa kwa kumdhalilisha Rais, Baraza la Mawaziri na majukumu yake katika serikali ya taifa chini ya sehemu 147 (1) na 152 (1) za katiba, Maseneta 28 waliunga mkono na 39 walipinga.
Kosa la latu lilikuwa ukiukaji wa sehemu za 6 (2), 10 (2)(a), 174, 186 (1), 189 (1) za katiba, ambapo alidhalilisha ugatuzi, Maseneta 19 waliunga mkono, 45 walipinga huku watatu wakisusia kupiga kura.
Kosa la nne ambalo ni ukiukaji wa sehemu ya 160 (1) ya katiba, Gachagua alishtakiwa kwa kuingilia uhuru wa majaji, Maseneta 51 waliunga mkono na 16 walipinga.
Katika kosa la tano,ambapo alidaiwa kukiuka sehemu za 3 (1) na 148 (5)(a) za katiba ambapo alikiuka kiapo cha afisi, Maseneta 49 waliunga mkono, 16 walipinga na wawili walisusia kupiga kura.
Maseneta 48 waliunga mkono, 18 walipinga na mmoja alisusia kupiga kura katika kosa la sita, ambapo alidaiwa kukiuka sehemu za 13 (1)(a) za katiba nasehemu ya 62 ya sheria za mshikamano na utangamano wa taifa.
Maseneta 13 walimpata na hatia ya uhalifu wa kiuchumi chini ya sehemu za 45 (1), 46, 47A (3) na sehemu ya 48(1) ya kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi, huku Maseneta 53 wakipinga na mmoja akisusia.
Katika kosa la nane ambapo anadaiwa kupotosha umma na kutoa matamshi ya uchochezi kinyume na sehemu ya 29 ya sheria za uongozi na maadili, Maseneta 27 waliunga mkono na 40 walipinga.
Kuhusu kosa la tisa ambapo anashtakiwa kwa kuishambulia idara ya ujasusi nchini na maafisa wake, Maseneta 46 waliunga mkono, 20 walipinga na mmoja alisusia kupiga kura.
Katika kosa la 10 ambapo anadaiwa kutomtii Rais ambaye ni kiongozi wa nchi na serikali, Maseneta 22 waliunga mkono na 44 walipinga.
Na hatimaye katika kosa la 11, ambapo Gachagua anadaiwa kuwadhulumu maafisa wa umma, Maseneta 17 waliunga mkono, 41 walipinga na wawili walisusia kupiga kura.
Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo la upigaji kura, Spika wa bunge la Senate Amason kingi alisema,” Bunge la senate limeamua kumuondoa afisni Rigathi Gachagua, Naibu Rais wa Kenya,”.