Marufuku ya mwanasheria Abdullahi: LSK yaikosoa Mahakama ya Juu

Martin Mwanje
2 Min Read

Siku moja baada ya Mahakama ya Juu kumpiga marufuku milele mwanasheria maarufu Ahmednasir Abdullahi kufika mbele yake, uamuzi huo umekosolewa na chama cha wanasheria nchini, LSK. 

Rais wa Mahakama ya Juu ambaye pia ni Jaji Mkuu Martha Koome aliwaongoza majaji wa mahakama hiyo katika kumuagiza mwanasheria Abdullahi kamwe kutofika mbele yao kutokana na hulka yake ya kuwashambulia mara kwa mara na kutilia doa maadili yao ya utendakazi.

Abdullahi amekuwa mstari wa mbele kudai kuwa uvundo wa ufisadi katika idara ya mahakama umefikia kilele.

“Kila mtu ana hiari ya kumchagua wakili anayemtaka. Mahakama haiwezi ikakiuka haki za wateja kwa kuchagua ni nani anayepaswa kufika mbele yake,” alisema mwenyekiti wa LSK Eric Theuri katika taarifa.

“Mahakama haina haki ya kisheria kumzuia wakili aliyeruhusiwa na LSK kuhudumu kama mwanasheria. Uamuzi huo hauna msingi kisheria, siyo halali, si wa kawaida na unaiashiria mahakama hiyo kama taasisi isiyokuwa ya haki.”

Theuri akiongeza kuwa uamuzi huo ukija wakati ambapo idara ya mahakama inashambuliwa kwa tuhuma za ufisadi, shutuma hizo basi zinastahiki.

LSK imekuwa mstari wa mbele kuitetea mahakama dhidi ya shutuma hizo, ambazo mwasisi wake ni Rais William Ruto.

Chama cha LSK kimeapa kupinga uamuzi huo kinaosema unaingilia mamlaka yake na kuitaka Mahakama ya Juu kuomba msamaha.

Share This Article