Msanii wa muziki wa Bongo Fleva nchini Tanzania Marioo ametambuliwa na kampuni ya Audiomack inayojihusisha na mauzo ya muziki mitandaoni, baada ya muziki wake kusikilizwa zaidi ya mara milioni 100.
Marioo ndiye wa tatu ambaye ameafikia ufanisi huo nchini Tanzania baada ya Diamond Platnumz ambaye muziki wake umesikilizwa zaidi ya mara milioni 168 na Harmonize ambaye ana streams zaidi ya milioni 121.
Tofauti na wawili hao wa kwanza, kampuni ya Audiomack iliamua kumtambua Marioo kwa njia ya kipekee pale ambapo maafisa wake walimwandalia tamasha na kumkabidhi bamba la ufanisi huo.

Akizungumza na wanahabari baada ya kukabidhiwa bamba hilo, Marioo alisema kwamba hatua hiyo inampa motisha wa kuendelea kwani ina maana kwamba kazi anazoandaa za muziki zinapendwa na wasikilizaji.
Mwanamuziki huyo alifichua kwamba mipango ya hafla hiyo ilikuwepo tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2025 na anaamini kwamba kampuni ya Audiomack ina mazuri kwa watanzania.
Kulingana naye, hakuna changamoto katika kuafikia utazamaji na usikilizaji wa kiwango cha juu mitandaoni na anaamini kwamba ataendelea kufanya vyema.
Alishukuru kwa fursa ambayo amepata ya kutumbuiza kwenye hafla ya tuzo za Trace kisiwani Zanzibar Februari 26, 2025.
Kuhusu ndoa ya Hamisa Mobetto na Aziz Ki, Marioo alisema amevutiwa sana lakini akashangaa alipoona Aziz akidondosha machozi.