Marekani yatahadharisha raia wake nchini Kenya kuhusu kemikali ya Cyanide

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya Marekani imetahadharisha raia wake walioko nchini Kenya wasipitie kwenye barabara ya kuu nambari A104 katika eneo la Kambembe huko Rironi, kaunti ya Kiambu kufuatia kumwagika kwa kemikali ya cyanide.

Raia hao wanashauriwa kutumia barabara mbadala ya Limuru na kutopitia barabara kuu ya Waiyaki na wafuatilie taarifa kufahamu iwapo eneo husika limesafishwa na ni salama.

Lori lililokuwa limebeba kemilaki hiyo ya cyanide lilihusika kwenye ajali na kusababisha kumwagika kwa kemikali hiyo barabarani na wakazi wanasemekana kuiiba.

Kemikali hiyo ni mbaya sana kwa binadamu na hata mazingira na inatambulika kama vidonge vidogo vya rangi nyeupe.

Wizara ya afya ilitoa tahadhari awali ikiwasihi watu wa eneo hilo kutopita karibu na eneo hilo kama njia ya kuhakikisha usalama wao.

Katibu wa afya ya umma Mary Muthoni alisema kwamba kumeza au hata kunusa kemikali hiyo ni hatari sana kwani inaweza kusababisha matatizo ya neva mwilini.

Huku hayo yakijiri mamlaka ya mazingira nchini NEMA, imeonya wote walioiba mitungi ya kemikali hiyo baada ya ajali na kwamba wanafaa kuitoa kwa vituo vya polisi vilivyo karibu nao.

Inaripotiwa kwamba mitungi kadhaa iliibwa na watu waliojitokeza baada ya lori lililokuwa limebeba kemikali hiyo lilihusika kwenye ajali na kuanguka Jumamosi huko Rironi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *