Marekani yaharibu meli ya Venezuela

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba jeshi la Marekani limeharibu meli ya venezuela inayodaiwa kuwa safarini kuelekea marekani ikiwa imebeba shehena ya mihadarti.

Kulingana na Trump wanaume watatu waliuawa katika shambulizi hilo dhidi ya kile anachokitaka kuwa makundi hatari ya ulanguzi wa mihadarati.

Rais wa Venezuela Nicolás Maduro alikuwa amesema awali kwamba nchi yake itajilinda dhidi ya uchokozi wa Marekani akimtaja mwanadiplomasia mkuu wa marekani Marco Rubio kuwa mkuu wa kifo na vita.

Mvutano kati ya nchi hizi mbili uliongezeka baada ya Marekani kuweka meli za kivita kusini mwa eneo la Karibea ikizitaja kuwa oparesheni za kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati huku ikitekeleza shambulizi ambapo watu 11 waliuawa.

Trump alitaja makundi ya ulanguzi wa mihadarati kuwa hatari kubwa kwa Marekani huku akichapisha video ya sekunde 30 inayoonyesha meli ikilipuka na kushika moto.

Baadaye tena katika afisi yake, Trump alisema kwamba Marekani ina ithibati na ushahidi kwamba meli iliyoharibiwa ilikuwa inamilikiwa na makundi ya kigaidi na walanguzi wa mihadarati.

“Unachohitajika kufanya ni kuangalia shehena, ilitapakaa kote baharini, mifuko mikubwa ya dawa aina ya cocaine na fentanyl kila mahali” alisema Trump.

Kiongozi huyo aliendelea kusema kwamba ulanguzi wa mihadarati hadi Marekani kupitia baharini umepungua kufuatia jitihada za hivi karibuni lakini akakiri kwamba bado mihadarati inaingizwa nchini humo.

Website |  + posts
Share This Article