Marekani na Uingereza zimefanya mfululizo mpya wa mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganai wa Houthi nchini Yemen.
Pentagon ilisema kuwa mashambulio ya Jumatatu yaligonga shabaha nane, ikijumuisha eneo la kuhifadhia chini ya ardhi na uwezo wa kudhibiti makombora wa Houthi.
Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamekuwa wakilenga meli wanazosema kuwa zina uhusiano na Israel na mataifa ya Magharibi zinazosafiri kupitia njia muhimu ya kibiashara ya Bahari ya Shamu.
Marekani na Uingereza zilisema zinajaribu kulinda “mtiririko huru wa biashara”.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Pentagon ilithibitisha “duru ya ziada ya mashambulio sawia na ya lazima” dhidi ya Houthis.
Taarifa hiyo iliongeza: “Lengo letu linabakia kupunguza mvutano na kurejesha utulivu katika Bahari ya shamu, lakini turudie onyo letu kwa uongozi wa Houthi: hatutasita kutetea maisha na mtiririko huru wa biashara katika moja ya nchi zenye nguvu zaidi ulimwenguni na njia kuu za maji katika uso wa vitisho vinavyoendelea.”
Hili ni shambulio la nane la Marekani dhidi ya wapiganaji wa Houthi nchini Yemen. Ni operesheni ya pili ya pamoja na Uingereza, baada ya mashambulizi ya pamoja kutekelezwa tarehe 11 Januari.
Taarifa hiyo ya pamoja ilisema mashambulizi hayo yalifanywa kwa msaada wa Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi.