Marais wa mataifa mbalimbali wawasili Nairobi kwa Kongamano la Tabia Nchi

Martin Mwanje
2 Min Read

Viongozi mbalimbali wa dunia wamezidi kutua katika jiji kuu la Kenya, Nairobi ili kuhudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi lililoanza jana Jumatatu. 

Kongamano hilo la siku tatu lilifunguliwa rasmi na Rais Willliam Ruto.

Anagalau Wakuu wa Nchi na Serikali 20 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo litakalomalizika kesho Jumatano.

Katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA, maafisa wakuu wa serikali walikuwa na shughuli si haba kuwapokea viongozi mbalimbali kutoka kila pembe ya dunia kuanzia jana Jumatatu jioni.

Miongoni mwao ni Marais Mohamed Yunusu al-Menfi wa Libya, Macky Sall wa Senegal na Suluhu Samia wa Tanzania.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo waliowasili nchini leo Jumanne asubuhi na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Alfred Mutua.

“Wakuu zaidi wa Nchi na Serikali wanatarajiwa kuwasili baadaye hii leo Jumanne asubuhi,” amesema Dkt. Mutua.

Wajumbe wapatao 30,000 wanahudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi na ambalo ni la kwanza kuwahi kufanyika.

Akilifungua kongamano hilo hapo jana, Rais Ruto aliwarai viongozi wa Afrika kuwekeza zaidi katika mitambo na mashine zinazotumia kawi safi na zisizochafua mazingira na pia kufanya kilimo bora kinachochangia pakubwa utunzaji mazingira.

“Mazungumzo ya Tabia Nchi yalianza mwaka 1992 mjini Rio De Janeiro brazil, ni miaka 31 baadaye ambapo kongamano hilo linaandaliwa Afrika kwa mara ya kwanza,” alisema Ruto.

“Tunao uwezo mkubwa wa kutumia kawi safi na malighafi asilia ambazo zinaweza kutumika vyema bila kuchafua mazingira lakini pia ni lazima tushirikiane kuondoa au kupunguza matumizi ya mashine na mitambo inayotoa gesi ya kabonidioksidi.”

Share This Article