Marais wa Kenya na Somalia wakutana, waunga mkono AUSSOM

Martin Mwanje
2 Min Read
Kenya na Somalia zimeunga mkono kuanzishwa kwa Misheni mpya ya Usaidizi na Uthabiti wa Somalia (AUSSOM).
Marais William Ruto wa Kenya na Hassan Sheikh wa Somalia wamesema AUSSOM itaipiga hatua kuelekea mbele kwa kutumia mafanikio ya mtangulizi wake, Misheni ya Mpito ya Umoja wa Afrika (ATMIS).
Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa mpito mzuri wa majukumu ya usalama kutoka ATMIS kuelekea AUSSOM, ambao umepangiwa kuanza Januari 1 mwakani.
Wamesisitiza kuwa ni lazima AUSSOM ipate ufadhili wa kutosha wakisema kuna haja ya kuangazia njia zote za ufadhili zinazoweza kutumika.
Rais Ruto na mgeni wake Rais Sheikh waliyazungumza hayo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa katika Ikulu ya Nairobi wakati wa ziara ya Rais huyo wa Somalia humu nchini.
Rais Sheikh alimpongeza mwenyeji wake kwa juhudi zake za kuhakikisha ujenzi wa taifa la Somalia na wajibu wake wa kurejesha amani na uthabiti katika taifa hilo la Upembe wa Afrika.
“Natambua wajibu mkubwa ambao Vikosi vya Ulinzi vya Kenya vimetekeleza katika kupambana na ugaidi pamoja na Vikosi vya Usalama vya Somalia na nchi zingine wachangiaji wa vikosi vya  ATMIS,” alisema.
Aidha viongozi hao waliangazia haja ya kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Usalama wa Vikosi vya Usalama vya Somalia (SSF).
Walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia kuimarisha uwezo huu na kuhakikisha mpito mzuri kuelekea AUSSOM.
Rais Ruto alimhakikishia mgeni wake kwamba Kenya inasimama bega kwa bega na Somalia na itaendelea kutoa usaidizi wote unaohitajika.
Share This Article