Marais Ruto, Mnangagwa waongoza mkutano wa kutafuta amani DRC

Martin Mwanje
2 Min Read

Marais William Ruto wa Kenya na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe jana Jumatano waliongoza Mkutano wa Pamoja Usiokuwa wa Kawaida wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Ruto ni mwenyekiti wa EAC huku Mnangagwa akiwa mwenyekiti wa SADC.

Mkutano huo, uliofanyika kwa njia ya mtandao, ulikusudia kuendeleza juhudi za kutafuta amani katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Wakati wa mkutano huo, Viongozi hao waliidhinisha uteuzi wa Rais wa zamani wa Botswana Mokgweetsi Masisi kujiunga na Jopo la Wapatanishi la wanachama watano lililopewa jukumu la kuongoza mazungumzo jumuishi mashariki mwa DRC.

Wanachama wengine wa jopo hilo ni Marais wa zamani Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Uhuru Kenyatta (Kenya), Catherine Samba-Panza (Jamhuri ya Afrika ya Kati) na Sahle-Work Zewde wa Ethiopia.

Aidha, viongozi hao waliidhinisha kuunganishwa kwa michakato ya amani ya Nairobi na Luanda kuwa mpangokazi mmoja wa upatanishi unaoongozwa na Afrika ukiungwa mkono na Umoja wa afrika, AU ili kuboresha uratibu na matokeo ya mpangokazi huo.

Pia waliidhinisha nyaraka muhimu za utenda kazi na mpango wa ukusanyaji rasilimali za kuendeleza mpango huo.

Wakati huohuo, mkutano huo ulielezea kufurahishwa na hatua zilizopigwa katika mipango ya kidiplomasia ya Washington na Doha na kuwapongeza Marais Paul Kagame wa Rwanda na Félix Tshisekedi wa DRC kwa kuridhia kufanya mazungumzo.

Walitambua juhudi zinazofanywa na Marekani na Qatar katika kutafuta amani kati ya Rwanda na DRC.

Rais Ruto aliunga mkono kwa dhati mtazamo wa mshikamano unaoongozwa na Afrika akisema hiyo ndio “njia ya uhakika” ya kuhakikisha amani na uthabiti wa kudumu mashariki mwa DRC.

Website |  + posts
Share This Article