Maono ya Mutahi Kagwe ya kilimo: sayansi, uendelevu na aliyojifunza kutoka kwa COVID-19

Marion Bosire
7 Min Read

Mteule wa wadhifa wa waziri wa kilimo Mutahi Kagwe, ameahidi kuleta mageuzi ya kilimo kupitia sayansi, kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabia nchi na kutumia aliyojifunza kutoka kwa COVID-19 kuleta mabadiliko halisi katika sekta ya kilimo.

Akizungumza mbele ya Kamati ya bunge kuhusu uteuzi chini ya uenyekiti wa Spika Moses Wetang’ula, iliyomsaili, Kagwe waziri wa zamani wa afya, aliwasilisha maono makubwa aliyosema yataleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini.

Kagwe alisisitiza umuhimu wa kutumia sayansi kuongoza sera za kilimo, kuhakikisha kwamba bidhaa zinazofika sokoni ni salama na endelevu.

Kauli yake ilijiri wakati ambapo mijadala imesheheni, kuhusu vyakula kisaki yaani GMO, mabadiliko ya tabia nchi na wasiwasi kuhusu ukosefu wa taarifa na sera zinazowekwa katika sekta ya kilimo.

Kuhusu suala nyeti la chanjo ya mifugo, Kagwe alisisitiza njia ya ushirikiano ili kuelimisha wakulima kuhusu hatua hiyo na kuwapa nafasi ya kufanya maamuzi sahihi kuhusu mpango huo wa serikali.

“Kuhusu chanjo ya mifugo, ni muhimu kuhusisha wadau wote muhimu na kuwapa taarifa sahihi. Uamuzi wa chanjo ya mifugo hatimaye utakuwa wa mmiliki. Wataalamu watashirikishwa kutoa ukweli na kushughulikia mitazamo potovu kuhusu chanjo hiyo,” alisema Kagwe.

Kikubwa katika maono ya Kagwe ni kupitishwa kwa sera zinazotegemea sayansi. Akizungumzia wasiwasi wa kimataifa kuhusu GMO, alisisitiza kuwa hakuna bidhaa itakayoruhusiwa chini ya uongozi wake bila uthibitisho wa kisayansi wa kina.

“Sisi sio wa kufanyiwa majaribio,” alisema Kagwe kwa uthabiti, akisisitiza kuwa Kenya haitakuwa uwanja wa majaribio ya bidhaa zinazozuiliwa kwingine.

“Hakutakuwa na bidhaa itakayouzwa katika nchi hii chini ya uangalizi wangu, katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, ambayo inajaribiwa hapa,” aliongeza, akithibitisha msimamo wake wa kulinda wakulima na watumiaji.

Namna Kagwe atatumia kutahadhari kuhusu GMO inahusishwa na mwelekeo mpana wa kilimo endelevu, hasa wakati Kenya inakumbwa na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabia nchi.

Mgogoro wa hali ya hewa duniani umesababisha kuanzishwa kwa kanuni mpya, ikiwemo sheria ya Umoja wa Ulaya kuhusu ukataji miti, ambayo inaweza kuathiri usafirishaji wa mazao ya Kenya nje ya nchi.

Ingawa alikubali changamoto zinazotokana na kanuni hizi, Kagwe alionyesha matumaini kwamba Kenya tayari iko mbele katika kuidhinisha mbinu za kilimo zinazowiana na mabadiliko ya tabia nchi, kama upanzi wa miti kando ya mashamba ya kahawa ili kuhifadhi mazingira.

“Sisi sio tu kwamba hatukati misitu ili kupanda mazao kama kahawa, bali pia tunapanda miti katika mashamba ya kahawa,” alisema Kagwe kwa fahari.

Akizungumzia wasiwasi kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kilimo, Kagwe alisisitiza haja ya mazao na mifugo inayoweza kustahimili ukame na joto linaloongezeka.

“Tunahitaji mazao yanayoweza kustahimili ukame, mifugo inayoweza kustahimili joto la juu na hali ya hewa ya joto,” alisisitiza, akiongeza kuwa maendeleo ya kiteknolojia, ikiwa ni pamoja na akili bandia, yatakuwa na jukumu muhimu katika utabiri wa hali ya hewa.

“Uwezo wetu wa kutabiri hali ya hewa utaendelea kuwa sahihi zaidi,” aliongeza Kagwe, akisisitiza jinsi uvumbuzi kama huo utawasaidia wakulima kujiandaa kwa mifumo ya hali ya hewa inayozidi kutokuwa ya kawaida.

Hata hivyo, mbinu ya Kagwe sio tu kuhusu sayansi na teknolojia; pia inahusisha masomo kutoka kwa mapambano ya Kenya na COVID-19.

Akikumbuka mikakati ya mawasiliano iliyotumika wakati wa janga hilo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na utoaji wa taarifa kwa wakati katika kusimamia majanga.

Kagwe alitaja kuwa wakati wa janga hilo, mawasiliano ya mara kwa mara yalikuwa muhimu katika kuwajulisha wananchi kuhusu hatari za kiafya na hatua za usalama.

“Tulikuwa na mkutano na vyombo vya habari kila siku, iwe ilikuwa mimi mwenyewe au wachezaji wengine au maafisa wa Wizara. Ilikubaliwa kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwasiliana nao,” alieleza.

Uzoefu huu umeunda mbinu yake ya kilimo, ambapo mawasiliano na ushirikiano na wadau, hasa wakulima, vitakuwa vya msingi. “Ng’ombe ni mali ya watu binafsi. Mahindi kwenye mashamba ni mali ya watu binafsi.

Sio mali ya serikali,” alisisitiza Kagwe, akielezea haja ya mbinu ya ushirikiano katika sera za kilimo. Alisisitiza kuwa kushirikisha wakulima, wataalamu, na wadau wengine ni muhimu kwa utekelezaji mzuri wa mageuzi ya kilimo.

Kagwe pia alionyesha wasiwasi kuhusu mfumo wa kodi wa kilimo nchini Kenya, ambao anaamini unazuia ukuaji wa sekta hiyo.

Kodi kubwa za bidhaa za kilimo, usafirishaji, na nyaraka zinaongeza mzigo mkubwa kwa wakulima na biashara.

“Ingekuwa bora kuunda kundi kubwa la wafanyabiashara na kuwa kodi kidogo, kuliko kuwa na wafanyabiashara wachache ambao unawatoza kodi kubwa,” alieleza Kagwe, akiahidi kuhimiza mageuzi yatakayofanya sekta hiyo kuwa rafiki kwa biashara.

Hatimaye, uteuzi wa Kagwe unadhihirisha mwelekeo mpya wa sera za kilimo za Kenya, mwelekeo unaojikita katika sayansi, uendelevu, na ushirikiano.

Akichukua masomo kutoka kwa janga la COVID-19, mbinu ya Kagwe inasisitiza umuhimu wa mawasiliano, haja ya kufanya maamuzi kulingana na data, na kulinda wakulima na bidhaa za kilimo za Kenya.

Wakati nchi ikijiandaa kwa mustakabali utakaosukumwa na mabadiliko ya tabia nchi, maendeleo ya kiteknolojia, na mabadiliko ya biashara ya kimataifa, uongozi wa Kagwe unaahidi kuwa ni chachu ya mwelekeo wa sekta ya kilimo ya Kenya.

Kamati ya Uteuzi inajumuisha Naibu Spika Gladys Boss, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah, Kiongozi wa Wachache Junet Mohamed, Naibu Kiongozi wa Wengi Owen Baya, Naibu Kiongozi wa Wachache Robert Mbui, Mbunge wa Tharaka George Murugara, Mbunge wa Kwanza Ferdinand Wanyonyi, Mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood, Mbunge wa Teso Kusini Mary Emase, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, Abdi Shuriye, Rahab Mukami, Dido Raso, Stephen Mule, David Pkosing, Nelson Koech na David Gikaria.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *