Maombi ya pasipoti yatakuwa yakichukuwa muda wa siku saba pekee kabla ya kupata stakabadhi hiyo muhimu ya usafiri.
Kulingana na Katibu wa Idara ya Uhamiaji Prof. Julius Bitok, serikali imefanya marekebisho kadhaa katika afisi za uhamiaji katika jumba la Nyayo, ikiwemo kuongeza muda wa kufanya kazi, kuwatimua mafisadi wote pamoja kuagiza mashine mpya za kuchapisha pasipoti.
Akizungumza mbele ya kamati ya bunge katika kaunti ya Mombasa, Prof. Bitok pia aliahidi kuwa wakatakamilisha maombi yote ya pasipoti ndani ya wiki mbili zijazo.
“Kumekuwa na pasipoti 100,000 ambazo hazijachapishwa na idadi hiyo tumeipunguza hadi 44,000 na tunatarajia kukamilisha idadi iliyosalia katika muda wa majuma mawili yajayo,” alisema Prof. Bitok
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki amefichua kuwa hazina kuu imetenga shilingi bilioni 1 nukta 3 kununua mitambo mipya ya uchapishaji ili kuharakisha mchakato wa kutoa vyeti hivyo.
Waziri alifanya ziara ya ghafla katika jumba la Nyayo jana Alhamisi jioni na kukutana na wafanyaikazi katika idara ya uhamiaji kama njia ya kuwatia moyo.
Wafanyakazi kadhaa waliokuwa wakihusika katika upokeaji hongo ya kati ya shilingi 2,000 na 5,000 ili kuwasaidia wanaotuma maombi kupata pasipoti kwa haraka wamekamatwa na kuhojiwa na maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai, DCI.
Wakenya wengi wamekuwa wakilalamikia ucheleweshaji wa kutoa kupata stakabadhi hiyo wengine ikiwachua hadi miezi mitatau kuipata.