Mamia ya Wapalestina wanahofiwa kufariki baada ya mlipuko mkubwa katika hospitali moja katika mji wa Gaza, unaolaumiwa na kundi la Hamas kwa shambulio la anga la Israel.
Jeshi la Israel limekanusha madai kuwa lilishambulia hospitali ya Al-Ahli Arab na kulaumu roketi ya Palestina.
Israel inasema mlipuko huo ulisababishwa na makombora yaliyorushwa vibaya na kundi jingine la Palestinian Islamic Jihad na pande zote mbili zinakana lawama.
Video iliyothibitishwa na BBC inaonekana kuonyesha hospitali hiyo ikiwaka moto.
Wafanyakazi wa dharura walihudumia majeruhi na kuwapeleka katika hospitali nyingine ya karibu.
Rais Joe Biden wa Marekani yupo safarini kuelekea nchini Israel kutafuta njia za kusuluhisha mzozo huo ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu.