Mkewe Rais Bi. Rachel Ruto alituzwa na taasisi ya Kalinga Institute of Social Sciences – KISS iliyoko Bhubaneswar, nchini India kutokana na mchango wake mkubwa katika kusaidia jamii.
Yeye ndiye mshindi wa tuzo ya usaidizi wa kibinadamu ya taasisi ya KISS mwaka 2022.
Katika hotuba yake ya kukubali tuzo hiyo, mkewe Rais aliapa kuendelea kusaidia jamii kwa kuendelea kutetea maslahi ya kina mama, watoto na makundi ya waliotelekezwa katika jamii kupitia kuhakikisha wanahusishwa kifedha, utunzaji wa mazingira, maisha bora na elimu.
Rachel alishukuru kwa tuzo hiyo akiitaja kuwa dhihirisho la kujitolea kwa watu wa taifa la Kenya.
Mama taifa alisema kwamba wakati huu ambapo dunia inakumbwa na changamoto nyingi, ni lazima watu wawe na umoja, wagawane raslimali ili kujenga dunia bora siku za baadaye.
Tuzo hiyo hutolewa na taasisi ya Kalinga ya sayansi ya jamii kutambua na kusherehekea watu ambao wamefanya vyema katika kutumikia binadamu ulimwenguni kote.
Tuzo hiyo ni alama ya matumaini, huruma na kujitolea na lengo lake ni kuhimiza watu wengine wengi kutoa huduma kwa jamii.