Mama taifa Rachel Ruto jana Jumatatu alizindua usambazaji wa chakula cha msaada kutoka kwa kampuni ya Soy Afriq, ikiongozwa na Mkurugenzi wake Cornelius Muthuri Mwega.
Chakula hicho kinajumuisha kilo 100,000 za unga wa uji ambao umeidhinishwa na Mpango wa Chakula Duniani, WFP.
Msaada huo unalenga kuwasaidia Wakenya ambao wanateseka kutokana na makali ya mafuriko yanayoshuhudiwa nchini, na kupiga jeki juhudi za serikali za kukabiliana na athari za mafuriko hayo.
Serikali kuu inasema kaunti 38 kati ya 47 zimeathirika na mafuriko.
Maeneo ambayo yameathirika na mafuriko ni pamoja na Mashariki, Kaskazini Mashariki na Ukanda wa Pwani.
Serikali imetenga shilingi bilioni saba kukabiliana na hali ya mafuriko inayoshuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi.