Mama Rachel ataka wanawake kujumuishwa katika masuala ya tabia nchi

Martin Mwanje
2 Min Read
Serikali za Afrika zimetakiwa kutekeleza sera ambazo zitahakikisha usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa nishati safi. 
Mkewe Rais Mama Rachel Ruto ametoa wito wa kujumuishwa kwa wanawake katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na ufadhili.
“Wanawake wanaweza wakatekeleza jukumu muhimu katika kutafuta masuluhisho ya mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Mama Rachel.
Alisema wanawake na watoto huathiriwa zaidi kutokana na uchafuzi wa mazingira licha ya kushiriki mipango ya nishati ya kijani.
Mama Rachel alitoa matamshi hayo wakati wa mkutano wa Wake wa Marais wakati wa Kongamano linaloendelea la Afrika kuhusu Tabia Nchi linaloendelea jijini Nairobi.
Alisema bara la Afrika lina idadi kubwa ya vijana duniani lakini ambao wana ujuzi mdogo katika kutumia fursa zilizopo za nishati ya kijani.
“Elimu huwezesha uelewa, ujuzi na uwezo wa kufikiri juu ya athari za tabia nchi,” alisema Mke wa Rais wa Sierra Leone, Bio.
Sawira Baumira, ambaye ni Mke wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Ghana, alisema madhara ya ikolojia yameathiri mamilioni ya wanawake barani Afrika.
“Hebu tuendeleze sera za ufadhili wa tabia nchi ambazo zinahakikisha usawa wa kijinsia,” alisema Mama Sawira.
Wengine waliokuwapo ni Mke wa Rais wa Burundi Angeline Ndayishimiye, Dimpo Masuku ambaye ni Mke wa Naibu Waziri Mkuu wa Eswatini na Mke wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Dorcas Rigathi.
“Wanawake ndio wanaochochea ukuaji wa uchumi; tunapaswa kubuni sera na hatua zinazowawezesha kukua katika sekta ya nishati,” alisema Dorcas.
Waziri wa Nishati Davis Chirchir alisema nishati safi ya kupikia ni mradi wa serikali ya Kenya.
“Tunapiga hatua katika kuunga mkono sera ambazo zinahakikisha ufadhili wa nishati safi; Rais ameahidi kuhakikisha kuwa gesi safi ya kupikia inapatikana,” alisema Chirchir.
Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa alitoa wito kwa nchi za magharibi kupunguza gesi chafuzi kwa mazingira ambazo hasa zinaathiri sekta za Afrika.
Alisema hatua zaidi na ufadhili wa wanawake utaboresha maisha ya wale walio chini kiuchumi.
Share This Article